Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
SERIKALI  imesema inafanyia kazi mpango mkubwa wa kupima ardhi zinazomilikiwa kimila na kutoa hati kwa wahusika.

Mpango huu ambao uko mbioni kuanza kama majaribio ni moja ya maazimio ya mkutano wa 9 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) uliomalizika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

Akitoa majumuisho ya mkutano huo kwa waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya TNBC, Balozi Ombeni Sefue alisema kuharakishwa kwa mpango wa kutoa hati za umiliki wa ardhi za kimila kutasaidia watanzania walio wengi zaidi kuweza kwenda katika vyombo vya fedha, kupata mikopo na kuboresha maisha.

Balozi Sefue ambaye pia ni Katibu Mkuu Kiongozi alisema tayari ofisi ya Mpango wa Kurasimisha Mali na Biashara Tanzania (MKURABITA) na Wizara ya Ardhi na Makazi zinaoanisha mifumo itakayowezesha mchakato huo kuwa wa haraka na gharama nafuu.

“Hatua hii itasaidia kupunguza gharama na watu wengi zaidi kufikiwa,” alisema, na kuongeza kuwa timu ya wataalamu kutoka serikalini itaundwa kushughulikia swala hilo.

Mpango huo utatumia vifaa na njia za kisasa na taarifa zote za ardhi zitaweza kupatikana kielektroniki.

Mapema, Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa TNBC alisema mpango huo utasaidia kuongeza thamani ya ardhi na kusaidia kuondoa migogoro ya ardhi hapa nchini.

Kwa mujibu wa Balozi Sefue utaratibu wa kuanzisha idara itakayosaidia ushiriki wa watanzania katika uwekezaji wa ndani na nje unaendelea.

Idara hiyo itakayokuwa katika Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) inalenga kujenga uwezo kwa watanzania na kuwafanya kuwa sehemu ya mchakato mzima ujenzi wa uchumi na sio kubaki kuwa watazamaji tu.

Mkutano huo pia uliongelea maswala mbalimbali yanayolenga kuimarisha mazingira ya biashara nchini na utalii.  Muda maalumu wa utekelezaji wa maswala hayo uliwekwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye alisema mkutano huo ulikuwa wa mafanikio.

“Hii inaonyesha kuwa sekta binafsi na umma zinaweza kufanya kazi pamoja kwa maendeleo ya nchi,” alisema.

Katibu Mtendaji wa TNBC, Bw. Raymond Mbilinyi alisema mkutano huo ulikuwa ni uthibitisho kuwa maendeleo yanaweza kupatikana kwa haraka kama sekta hizo zitafanya kazi kwa ushirikiano wa dhati.

Wakati wa mkutano huo, Rais Kikwete alizindua mfumo wa kielektroniki wa usajili wa majina ya biashara.

Mfumo huo ulioanza kutumika na wateja wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) mwezi wa Sita mwaka huu unamwezesha mwananchi kupata jina la biashara ndani ya dakika kumi tu kama kila kinachohitajika kipo.

Mkutano huo ulikuwa wa mwisho kuendeshwa na Rais Kikwete kama Mwenyekiti wa TNBC kabla ya kumalizika kwa muda wake wa uongozi mwaka huu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. Ningependa kuwakumbusha jicho lenu liangaze nako upande wa wale wanaomiliki maelfu ya hekta za ardhi hili nalo mngeliweka ktk mpango maalum wa kuruhusu kiasi fulani tu cha ardhi kumilikiwa na mtu mmoja mmoja. Mfano haiingi akilini mtu mmoja kumiliki zaidi ya hekali 5000 za ardhi ktk mkoa mmoja kisha mtu huyohuyo ana mashamba na majumba ktk mikoa mingine.Najua hili ni gumu kutendeka lakini kwa sababu zilizo wazi ambazo kila mtu anazifahamu ila kukumbushana ni wajibu.

    ReplyDelete
  2. Mdau hapo juu umenena. tena unakuta hayo maelfu ya hekari yana hati miliki lakini mwananchi anayemiliki eneo la miguu 20x20 madale au msakuzi kupata hati ni changamoto so suala la kutumia ardhi ili kupata mikopo na kuboresha maisha litanufaisha ambao tayari maisha yao ni bora wale tunaostahili kuboresha maisha hati za viwanja hatuna na tumekata tamaa ya kuzipata.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...