Na Greyson Mwase, Handeni-Tanga

Wachimbaji wa madini nchini wametakiwa kuendana na teknolojia inayokua kila kukicha ili kuwezesha sekta ya madini kuwa na mchango zaidi katika pato la taifa.

Rai hiyo ilitolewa na Afisa Madini Mkazi kutoka Ofisi ya Madini- Handeni mkoani Tanga, Frank Makyao kwenye ufunguzi wa mafunzo juu ya matumizi ya huduma za leseni za madini kwa njia ya mtandao yaliyokutanisha wachimbaji wa madini katika kanda ya mashariki yanayoendelea mjini Handeni.

Lengo la mafunzo hayo lilikuwa ni kuwapa uelewa wa matumzi ya huduma za leseni za madini kwa njia ya mtandao ijulikanayo kama online mining cadastre transactional portal.

Makyao alisema kuwa ni vyema wamiliki wa leseni za madini wakaachana na mfumo wa zamani wa kutumia makaratasi katika huduma za leseni kwani mfumo wa kisasa wa huduma za leseni kwa njia ya mtandao utawawezesha kupata leseni kwa wakati na uwazi zaidi.

“ Kwa mfano kuanzia sasa mtaweza kufanya malipo ya leseni zenu kwa njia ya M-Pesa, Airtel Money na Tigo Pesa hali itakayowezesha ofisi za madini kupata mapato zaidi.” Alisisitiza Makyao

Makyao aliendelea kusema kuwa wachimbaji wa madini wanatakiwa kuchangamkia mafunzo yanayotolewa na wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini na kuanza kutumia huduma hiyo mara moja ili kurahisisha utendaji wao wa kazi.

Alisema biashara katika nchi nyingi duniani imekuwa ikifanyika kwa njia ya mtandao na kuwataka wachimbaji wa madini kuchangamkia fursa hiyo ili waweze kuendana na ushindani wa biashara ya madini duniani.

Aidha aliwataka wachimbaji wa madini kufuata sheria za madini katika uombaji na umiliki wa leseni za madini pamoja na kushirikiana na serikali kwa kulipa kodi na tozo mbalimbali kama Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 inavyowataka ili sekta hiyo iwe na mchango zaidi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Afisa Madini Mkazi- Ofisi ya Madini Handeni, Frank Makyao (kulia) akifungua mafunzo kuhusu huduma za leseni za madini kwa njia ya mtandao yaliyokutanisha wachimbaji wa madini kanda ya mashariki mjini Handeni. Kutoka kushoto ni wawezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Pendo Elisha na Charles Gombe.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Charles Gombe (kushoto) akisisitiza jambo katika mafunzo hayo. Kulia ni Afisa Madini Mkazi- Ofisi ya Madini Handeni, Frank Makyao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...