Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akipokea hundi ya shilingi milioni 80 kutoka kwa Balozi wa Pakistan nchini, Amir Khan  (wapili kushoto ukiwa ni mchango  kwa waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani  Kagera. 
Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye hoteli ya Kyatt Regency jijini Dar es salaam Septemba 30, 2016. Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje na  Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Augustine Mahiga na  kulia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya Shilingi milioni 50 kutoka kwa Mwakilishi Mkazi wa Tasisi ya Aga khan nchini, Amin Kurji (kulia) ukiwa ni mchango kwa waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera. Makabidhiano hayo yalifanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam Septemba 30, 2016. Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje na  Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Augustine Mahiga na wapili kulia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako. 
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea jumla ya sh. milioni 190 kutoka kwa balozi wa Pakistan nchini Mhe. Amir Khan, Kaimu Balozi wa China Mhe. Gou Haodong na Taasisi ya Aga Khan.

Fedha hizo zimetolewa ili kusaidiia  wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera Jumamosi, Septemba 10, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 17 na wengine 440 walijeruhiwa.

Pia tetemeko hilo limesababisha nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi baada ya kupata nyufa na 9,471 zimepata uharibifu mdogo huku wananchi 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.

Makabidhiano ya michango hiyo, yamefanyika leo (Ijumaa, Septemba 30, 2016) kwenye Hotel ya Hyatt Regency jijini Dar Es Salaam ambapo Waziri Mkuu aliwashukuru kwa michango hiyo na alitumia fursa hiyo kuwaomba wale walioahidi kutoa michango wakamilishe ahadi zao.

“Ninawaomba wale walioahidi kutoa michango wakamilishe ahadi kwa kuzileta ofisini kwangu au kutuma kupitia akaunti ya maafa iliyofunguliwa katika Benki ya CRDB yenye Namba. 015 222 561 7300 kwa jina la KAMATI MAAFA KAGERA – Swiftcode: CORUtztz,” amesema.

Amesema watu walio mbali na benki watumie namba za simu zilizotolewa mahsusi kwa ajili ya kupokea michango ya maafa hayo ambazo ni 0768-196-669 (M-Pesa), au 0682-950-009 (Airtel Money) au 0718-069-616 (Tigo Pesa).

Akikabidhi hundi kwa Waziri Mkuu, Balozi wa Pakistan, Mhe. Amir alisema wanaamini mchango huo wa sh. milioni 80 walioutoa utasaidia kuwapunguzia uchungu wananchi wa Kagera kutokana na athari zilizosababishwa na tetemeko la ardhi.

Kwa upande wake Kaimu Balozi wa China Mhe. Haodong alimweleza Waziri Mkuu kwamba wameshtushwa na tukio hilo na tayari walishawapeleka madaktari na wataalamu wengine mkoani Kagera na leo walikuwa wanakamilisha ahadi yao ya kutoa mchango wa sh. milioni 60.
Naye Muwakilishi Mkazi wa Taasisi za Aga Khan nchini, Amin Kurji  alimkabidhi Waziri Mkuu hundi ya sh. milioni 50.                               
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
IJUMAA, SEPTEMBA  30, 2016.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...