Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 30 Septemba, 2016 amefunga maadhimisho ya miaka 52 ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa kushuhudia zoezi la medani liitwalo ''Amphibious Landing'' lililofanyika katika Kijiji cha Baatini Wilaya ya Bagamoyo. Mkoani Pwani.
Zoezi hilo lililochukua muda wa wiki mbili, limeshirikisha kamandi zote tano za JWTZ  ambazo ni Nyika, Majini, Anga, Kamandi ya Makao Makuu na  Jeshi la Kujenga taifa limefanyika katika ufukwe wa bahari ya Hindi na limetekelezwa kwa mfano wa mapambano ya kivita yaliyohusisha kutua nchi kavu kutoka majini na kukomboa eneo lililotekwa.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa zoezi hilo Rais na Amiri jeshi Mkuu Dkt.John Pombe Magufuli amempongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange pamoja na Makamanda na Wapiganaji wote wa JWTZ walioshiriki katika zoezi hilo ambalo limefanywa kwa umakini, uhakika na weledi wa hali ya juu.
''Kwa kweli nimefurahi na nimeamini tuna wapiganaji wa kutosha katika maeneo yote, hii mikakati na mipango iliyotumika inaonesha tuna jeshi imara na linaloaminika'' amesema Dkt. Magufuli.  
Rais na Amiri Jeshi Mkuu amewahakikishia Makamanda na Wapiganaji wote wa JWTZ kuwa Serikali yake itahakikisha inaendeleza na kuongeza zaidi juhudi zilizofanywa na Marais waliopita kwa kuimarisha na kuwa na jeshi la kisasa linalotumia vifaa na teknoljia ya kisasa na pia itahakikisha maslai ya askari yanaboreshwa.
Aidha, Dkt. Magufuli ametaka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuimarishwa zaidi na kujielekeza katika uzalishaji mali ikiwemo uwekezaji katika viwanda.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein ambaye pamoja na kuipongeza  JWTZ amesema miaka 52 tangu kuanzishwa kwa Jeshi hilo Watanzania wanashuhudia jeshi lao likiwa imara na makini zaidi kwa ajili ya kulinda nchi.
Nae Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange amemshukuru Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada zake na nia yake ya kuliimarisha Jeshi na kuboresha maslai ya Makamanda na Wapiganaji na ameongeza kuwa anajivunia kuwa kiongozi  wa Jeshi hilo.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Viongozi wengine wakiwemo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Zanzibar Abdulhamid Yahaya Mzee.
Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli, amemuagiza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange kuwapa ajira za JWTZ askari mgambo wote walioshiriki zoezi la Amphibious Landing.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam.
30 Septemba, 2016
Amiri  Jeshi Mkuu Rais Dkt John Pombe Magufuli akipiga ngoma za bendi ya jeshi ya Mwenge Jazzz wana Paselepa wakati  wa kufunga Zoezi la medani katika kilele cha maadhimisho ya miaka 52 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) huko Baatini, Bagamoyo mkoa wa Pwani leo Septemba 30, 2016
 Amiri  Jeshi Mkuu Rais Dkt John Pombe Magufuli, Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein na meza kuu wakipiga saluti wakati wa wimbo wa Taifa wakati wa kufunga Zoezi la medani katika kilele cha maadhimisho ya miaka 52 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) huko Baatini, Bagamoyo mkoa wa Pwani leo Septemba 30, 2016
 Ndege vita zikipita angani katika kilele cha maadhimisho ya miaka 52 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) huko Baatini, Bagamoyo mkoa wa Pwani leo Septemba 30, 2016
 Vifaru vinavyopita baharini na nchi kavu vikiwa katika zoezi la "Ambhibious Landing"  katika kilele cha maadhimisho ya miaka 52 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) huko Baatini, Bagamoyo mkoa wa Pwani leo Septemba 30, 2016
Amiri  Jeshi Mkuu Rais Dkt John Pombe Magufuli, Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein na meza kuu wakipiga makofi wakati wa Zoezi la medani katika kilele cha maadhimisho ya miaka 52 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) huko Baatini, Bagamoyo mkoa wa Pwani leo Septemba 30, 2016. PICHA NA IKULU.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...