Teresia
Mhagama na Mohamed Saif
BENKI ya Dunia (WB)
imeahidi kutoa Dola za Marekani milioni 4 sawa na zaidi ya shilingi Bilioni 8, kwa
ajili ya Ruzuku katika shughuli za
uchimbaji mdogo wa madini nchini.
Hayo yamebainishwa hivi
karibuni jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
mara baada ya kumaliza kikao na watendaji Wakuu wa Benki ya Dunia wanaosimamia
Miradi ya Sekta ya Madini.
Profesa Muhongo alisema
kuwa sehemu ya fedha hizo za Ruzuku ambayo ni ya Awamu ya Tatu zitatolewa mwezi
Septemba, 2016.
Aliongeza kuwa fedha hizo
zitatumika kufadhili uendelezaji wa vituo Saba vya mfano vya utafutaji na
uchimbaji mdogo wa madini ambavyo vitachaguliwa na Wizara baada ya kufanya
tathmini ya maeneo yanayoweza kuwekwa vituo hivyo.
“Sio hivyo tu, Fedha
hizi za Benki ya Dunia zinalenga kuwafadhili wanawake kwenye shughuli za
uchimbaji mdogo wa madini, ukataji na uchongaji wa madini ya vito ili idadi ya
wanawake wanaojishughulisha na Sekta ya Madini iongezeke,” alisema Profesa
Muhongo.
Aidha, Profesa
Muhongo alitoa wito kwa wataalam wote wanaosimamia miradi inayofadhiliwa na
Benki ya Dunia katika Sekta ya Madini kuhakikisha kuwa utekelezaji wa miradi
hiyo uende kwa kasi ili kuleta matokeoyaliyotarajiwa.
Benki
ya Dunia kupitia Wizara ya Nishati na Madini imeendelea kutoa Ruzuku katika Uchimbaji
madini mdogo ambapo katika mwaka wa Fedha 2015/16 zilitengwa takribani Shilingi
bilioni 7.2 ambazo zilitolewa kwa vikundi 111 vya wachimbaji wadogo na watoa
huduma mbalimbali katika sekta ya uchimbaji madini mdogo.
Vilevile,
katika mwaka wa Fedha 2013/2014, Fedha za Ruzuku zilizotolewa kwa Wachimbaji
Wadogo zilikuwa ni Dola za Marekani 500,000 sawa na takribani Shilingi Bilioni 1
zilizotolewa kwa waombaji 11. Fedha hizi ziliwalenga wachimbaji madini wadogo
pekee tofauti na awamu zilizofuata.
Utoaji huo wa Ruzuku unaenda
sambamba na utoaji wa elimu na mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini
waliopata ruzuku husika ili kuhakikisha kuwa shughuli zilizopata ufadhili
zinaleta tija.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...