Na Lilian Lundo-MAELEZO
Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Mhe. Said Meck Sadiki amesema zoezi la usafi wa mazingira litakalofanyika siku ya Maadhimisho ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe 9 Desemba, litakuwa ni endelevu kwa mkoa wa Dar es Salaam hata baada ya kumalizika kwa maadhimisho hayo.

Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Tano. Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli aliagiza kuwa Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Tanzania Bara mwaka huu yatumike kwa kufanya usafi wa Mazingira kote nchini badala ya kufanya sherehe za gwaride la askari wa vikosi vya Ulinzi na Usalama.

Akiongea na vyombo vya habari leo Mhe. Sadiki alianza kwa kumpongeza Mhe. Rais kwa uamuzi aliouchukua wa kubadilisha sherehe za uhuru kuwa ni siku ya kufanya kazi badala ya kwenda uwanjani na kuangalia gwaride na halaiki mbalimbali kama ilivyokuwa ikifanyika miaka iliyopita.

“Mhe. Rais katurejesha kule tulipotoka ambako kauli mbiu ya sherehe za uhuru ilikuwa ni uhuru na kazi au uhuru ni kazi wakati watanzania walikuwa wakiungana na kufanya kazi kwa umoja na kushirikiana,” alisema, Mhe. Sadiki.

Aidha, Mhe Sadiki alisema, zoezi la usafi kwa mkoa wa Dar es Salaam litaanza rasmi tarehe 1 Disemba mwaka huu na kumalizikia 9 Disemba mwaka huu siku ya kilele cha maadhimisho ya siku ya uhuru na kuongeza kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu.

Mhe. Sadiki aliongeza kwa kusema kuwa, uongozi wa mkoa umewaomba wadau kujitokeza kwa kuchangia fedha au vifaa kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo na amewataka watendaji kushawishi wananchi wa maeneo yao kutafuta vifaa badala ya kusubiri kuletewa na Halmashauri.

Pia, Mhe Sadiki amewahimiza watendaji wa mitaa na kata kutimiza wajibu wao wa kuhakikisha maeneo wanayoyasimamia yanakuwa katika hali ya usafi muda wote ili kuepukana na magonjwa ya mlipuko na pale inakapobainika eneo fulani lipo katika mazingira ya uchafu basi mtendaji wa eneo hilo atawajibishwa kwa kufikishwa katika vyombo vya sheria kwa kosa la kutotimiza wajibu wake. 


Vilevile ametoa wito kwa wananchi kuzingatia usafi kwa kuacha tabia za kutupa taka ovyo hasa wanapokuwa katika vyombo vya usafiri na kutokujisaidia katika mitaro au vichaka ili kuepukana na uchafuzi wa mazingira kunakopelekea kutokea kwa magonjwa ya mlipuko.


Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Mhe. Said Meck Sadiki akizungumza na waandishi wa habari ( hawapo pichani) ofisini kwake leo alipokuwa akizungumzia zoezi la usafi na namna mkoa ulivyojipanga kutekeleza zoezi hilo siku ya 9 Disemba.

Waandishi wa habari wakifuatilia kwa makini maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam juu ya usafi wa mazingira siku ya 9 Disemba.


Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Raymond Mushi (Kulia) akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Said Meck Sadiki (Kushoto) alipokuwa akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu utekelezaji wa agizo la Mhe Rais la kufanya usafi wa mazingira katika maadhimisho ya sherehe za uhuru wa Tanzania Bara. (Picha zote na Raymond Mushumbusi – Maelezo ) 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. The mdudu, kwa kasi ya mpendwa wetu Magufuli viongozi wengi wa JIJI la DAR lazima mta fukuzwa kazi mimi nilijua mtatunga sheria za usafi ambazo ni lazima kuzifuata lakini maneno matupu kama haya mshasema sana pasipo na utekelezaji ndugu zangu amkeni kwenye usingizi mzito kwa jinsi utendaji kazi wa Magufuli mtatia akili nyie wote wazembe mulio zoea kuzunguuka na viti ofisini sasa mtaviona vichungu na wengi wenu mtaacha kazi wenyewe kwa sababu hamjui nini maana ya uongozi na nini maana ya kazi #mavidebe hongera sana rais Magufuli

    ReplyDelete
  2. Kufanya usafi wa miji si tatizo, bali ukusanywaji wa taka ndiyo tatizo kubwa, naona serikali iandae utaratibu wa ukusanywaji wa taka ili zitumike katika mambo mengine ya maendeleo k.m.(mbolea, ufuaji wa umeme n.k) badala ya taka hizo kuzagaa kwenye majalala na kuchafua mazingiria husika.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...