Na Joseph Ishengoma, MAELEZO
Askofu Mkuu wa jimbo kuu la Tabora Mhashamu Paulo Ruzoka (pichani) kesho (tarehe 27.11.2015) anatarajia kuongoza ujumbe wa Tanzania kwenye ziara ya Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani Baba Mtakatifu Francis nchini Uganda.
Baba Mtakatifu Francis anatarajia kuwasili nchini Uganda kesho kwa ziara ya siku mbili akitokea Kenya kabla ya kuelekea Afrika ya Kati.
Hii ni ziara ya kwanza kwa kiongozi huyo Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani kutembelea Bara la Afrika tangu alipoliongoza Kanisa Katoliki mwaka 2013.

Katibu wa Baraza la Maaskofu (TEC) nchini Padre Raymond Saba amesema  Mabaraza ya Maaskofu ya Kenya na Uganda kwa pamoja yalitoa mwaliko kwa TEC kushiriki katika ziara ya Baba Mtakatifu katika nchi hizo.

“Tulipata mwaliko kutoka Kenya na Uganda, lakini tumeangalia nafasi yetu na jinsi ya kushiriki katika ziara hii. Hatukuweza kutuma mwakilishi Kenya, lakini Askofu Ruzoka ataiwakilisha TEC Uganda,” amesema.
Kwa mujibu wa msemaji huyo, jana mabasi mawili ya waumini wa dini ya Kikristo yaliondoka mjini Mwanza kuelekea Namugongo, Uganda ambapo Baba Mtakatifu atakapofanyia ibada.
Eneo la Namugongo ndipo Mfalme Kabaka Mwanga II alipowachoma na kuwaua mashahidi 22 wa Uganda waliofia dini katika karne ya 18.
“Natoa wito kwa waumini wa Kanisa Katoliki nchini, wafuatilie na kusikiliza kwa makini ujumbe wa Baba Mtakatifu aliouleta katika Barani Afrika kwa sababu unagusa moja kwa moja amani na ushirikiano miongoni mwa jamii,” amesema.
Kwa mujibu wa Padre Saba, Baba Mtakatifu hufanya ziara kufuatia mwaliko wa kanisa na serikali ya mahali husika au tukio la kimataifa linalohusiana na imani Katoliki.
Amesema, “Kanisa pekee yake haliwezi kufanikisha ziara ya Baba Mtakatifu. Ndio maana alipofika Kenya alipokelewa na Rais Uhuru Kenyatta na hata alipokuwa Marekani alipokelewa na Rais Baraka Obama ingawa sio rahisi kwa kiongozi wa Marekani kumpokea mgeni uwanja wa ndege.”  
Ziara ya Baba mtakatifu nchini Marekani ilipangwa kabla hajawa kiongozi Mkuu wa kanisa Katoliki. Ziara hiyo ilitokana na kongamano la kimataifa la familia lililofanyika mjini Philadelphia.
Papa Francis anatarajia kuhudhulia kongamano la vijana ulimwenguni nchini Poland mwaka 2016.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...