Na Lydia Churi-NEC
TUME ya Taifa ya Uchaguzi imewataka wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini ambao ni wasimamizi wa Uchaguzi kuhakikisha wanakagua vifaa wanavyopokea vinavyosambazwa hivi sasa kwa ajili ya Uchaguzi ili kuondoa dosari zinazoweza kujitokeza wakati wa Uchaguzi Mkuu. 

Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Eliudi Njaila ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam wakati wakiwaonyesha waandishi wa habari karatasi za mfano za kupigia kura zilizopokelewa na NEC kwa ajili ya kuanza kusambazwa nchini kote.

Njaila amesema karatasi hizo za kupigia kura zitakapowafikia wakurugenzi wa Halmashuri wazikague na hasa kuangalia nembo ya NEC kama ipo sahihi pia waangalie majina ya wagombea na vyama wanavyoviwakilisha kama viko sahihi na vinakidhi mahitaji ya majimbo yao ya Uchaguzi.

 Aidha aliongeza kuwa karatasi hizo za kura zitasambazwa katika kata zote ambapo kila kata itapewa karatasi za mfano wa kupigia kura 200 na zitagawiwa kwa wagombea wa ngazi  zote ili wawaelimishe wanachama wao namna ya kupiga Kura na kuonyesha mgombea yupo katika namba ipi kama ilivyoonyeshwa katika karatasi hizo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi wa NEC, karatasi hizo za mfano wa kupigia Kura kwa ajili ya wagombea wa Urais, Ubunge na Udiwani zitasambazwa kuanzia sasa na ifikakapo Oktoba 7 zitakuwa zimeshafikishwa nchi nzima.

Tume imekuwa ikiendelea kupokea vifaa mbalimbali kwaajili ya Uchaguzi Mkuu na Mara vinapowasili katika ofisi za Tume vinasafirishwa na kupelekwa katika majimbo yote ya Uchaguzi nchini. Hadi sasa vifaa vyote vimekwisha sambazwa isipokuwa karatasi halisi za kupigia kura ambazo zitasambazwa siku chache kabla ya siku ya Uchaguzi. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...