Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Dkt. Neema Rusibamayila toka Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) mapema hii leo jijini
Dar es Salaam kuhusu maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji inayotarajiwa kuanza Agosti Mosi
hadi Saba ambapo kitaifa itafanyika mkoani Dodoma.
Na. Eliphace Marwa – Maelezo.
Katika kuzingatia na kuboresha afya ya mtoto, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeendelea
kuwahimiza wanawake kuzingatia utunzaji na ustawishaji wa watoto kwa kuwapa haki ya
kunyonya maziwa ya mama.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Dkt. Neema Rusibamayila amesema wakati
Tanzania inategemea kuungana na mataifa mengine duniani ni vema jamii ikatambua umuhimu
wa lishe kwa mtoto.
“Jamii inapaswa kutambua umuhimu wa unyonyeshaji maziwa ya mama pekee katika miezi sita
ya mwanzo ya maisha ya mtoto na kuendelea kunyonyeshwa mpaka umri wa miaka miwili au
zaidi” alisema Dkt. Neema.
Kwa upande wa mtoto, Dkt. Neema alisema maziwa hayo yana faida nyingi ikiwemo kumpatia
virutubisho vyote anavyohitaji kwa uwiano sahihi kwa afya na ustawi kwani viini vya
kingamwili vinavyofanya kazi kama chanjo dhidi ya maradhi humeng’enywa na kufyonzwa
kirahisi zaidi mwilini tofauti na vyakula vingine.
Aidha aliongeza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yataenda sanjari na kilele cha maadhimisho
ya miaka 25 ya Azimio la Innocenti la mwaka 1990ambalo linasisitiza umuhimu wa kulinda,
kuendeleza na kusaidia unyonyeshaji na ulishaji bora wa watoto.
Mgeni rasmi katika Maadhimisho hayo yanayotarajiwa kuanza Agosti Mosi na kufikia kilele
chake Agosti 7 mkoani Dodoma katika viwanja vya Nanenane ni Waziri wa Afya na Ustawi wa
Jamii Dkt. Hussein Mwinyi yakiwa na kauli mbiu “Unyonyeshaji na kazi, hakikisha
inawezekana” yenye lengo la kuwasaidia wanawake wote wenye ajira rasmi na zile zisizo rasmi
waweze kutunza watoto wao ipasavyo pasipo kuathiri ajira zao zinazowapatia kipato.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...