Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watuhumiwa
watatu raia wa kigeni kwa makosa yanayohusiana na wizi wa mtandao kwa lengo la
kuiba katika vyombo vya fedha kama
mabenki, maduka ya kubadilishia fedha (Bureau de Change) au kuingilia miamala
ya fedha zinazosafirishwa na wateja kutoka nje na ndani ya nchi.
Polisi wa kikosi Maalum cha kupambana na wizi wa mtandao (Cyber Crime)
walipata taarifa za kuaminika kwamba watu hao watatu walikuwa katika mazingira
ya kutiliwa mashaka na ndipo Polisi walienda Mtaa wa Mindu eneo la Upanga na
kuwakamata. Watu hao walikutwa katika nyumba namba 416 iliyopo katika ghorofa
ya nne na walitambuliwa kwa majina yafuatayo:
1.
FOTIOS S/O
VOGIATZIS, Miaka 32, Mfanyabiashara, Mkazi wa Upanga, Raia wa nchini UGIRIKI mwenye
Passport namba AK2669977.
2.
ATHANASIOS
S/O VOGIATZIS, Miaka 30, Mfanyabiashara, Mkazi wa Upanga, Mkazi wa Ugiriki
mwenye Passport namba AK3049876.
3.
PANAGIOTIS
S/O ANGELIDIS, Miaka 25, Mkazi wa
Upanga, Raia wa UGIRIKI mwenye Passport namba AK2644930.
Watu hao watatu ambao ni raia wa nchini Ugiriki kumbukumbu zao
zinaonyesha kwamba wamekuwa wakiingia na kutoka nchini Tanzania na kwenda nchi
mbalimbali za Afrika na Ulaya katika namna ambayo inaonyesha kuwa ni wahalifu
wa kimataifa kupitia mitandao.
Katika upekuzi watu hao wamekamatwa na vielelezo mbalimbali
vinavyopashiria njama zao kama ifuatavyo:
1. Muhuri mmoja wa kughushi ulioandikwa “Inspector
General of Police DSM”
2. Nyaraka mbalimbali za kughushi za Polisi Tanzania
zinazowasaidia kwa lengo la kupata
malipo ya bima nje ya nchi ambazo zina mihuri ya kughushi.
3. Zimepatikana Kompyuta Mpakato (Laptops) zipatazo
tisa ambazo watuhumiwa hawa huzitumia kwa ajili ya mawasilisano pamoja na
uhalifu huo wa kimataifa.
4. Zimekamatwa laini za simu za mkononi (Cheap) za
kampuni ya simu ya Airtel ambazo baadhi zimetumika na nyingine hazijatumika.
5. Aidha, zimekamatwa kadi mbalimbali za benki
(Credit Cards) zipatazo 13 zinazotumika kutoa fedha, kuingiza fedha, au
manunuzi mengine za ATM.
Pia watuhumiwa hao wamekamatwa na vitabu vitano vyenye kumbukumbu za
majina, anwani, pamoja na namba za siri za wateja mbalimbali wa mabenki
mbalimbali kutoka nchi za Tanzania, Zambia, Afrika Kusini, Kenya, Uingereza na Nigeria.
Uchunguzi ziadi unaendelea kuhusu raia hao watatu kutoka nchi ya
Ugiriki ili kubaini mtandao wao na kugundua matukio mbalimbali ambayo
wameyafanya.
TAHADHARI KWA WANANCHI NA WAGENI WENGINE
Pamoja na kuibuka na wimbi hili la wezi wa mtandao bado ni salama
kuweka na kutoa fedha katika mabenki hapa nchini. Hata hivyo kutokana na wimbi
hili la wizi kwa njia ya mtandao, ni muhimu sasa kuzuia uhalifu wa aina hii kwa
ushirikiano kati ya wamiliki wa mabenki
na wateja wao.
Jeshi la Polisi
linashauri (pamoja na maelekezo mengine ya benki) njia sahihi ya kwanza ya
kuzuia ni kuhakikisha kwamba miamala yote inayofanyika katika akaunti za benki
ni lazima ifahamike kwa mteja kwa njia zifuatazo:
1.
Mteja
ajulishwe kwa simu ya mdomo ili kuthibitisha muamala.
2.
Mteja
atumiwe ujumbe kwa kila muamala unaofanyika kupitia ujumbe mfupi wa maandishi (SMS)
kumjulisha mteja kiasi kilichotolewa, kiasi kilichoingizwa au makato au
maingizo yoyote kwa muda ule ule.
Aidha tunawaomba wananchi waendelee kushirikiana na Jeshi la Polisi na
wasikubali kutoa nambari za akaunti zao kwa watu wasiohusika au nambari zao za
siri hata kwa mtu ambaye ni ndugu wa karibu sana.
Mara baada ya upelelezi kukamilika watuhumiwa hao watafikishwa
mahakamani.
S. H. KOVA,
KAMISHNA WA
POLISI KANDA MAALUM,
DAR ES SALAAM.
DAR ES SALAAM.
Hawa wageni wasituletee washtakiwe
ReplyDelete