Na Mwandishi wa Wizara
ya Mambo ya Nje.
Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wameanza kikao cha siku mbili jijini Harare, Zimbabwe leo kufanya matayarisho ya Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo, utakaofanyika hapo tarehe 29 Aprili, 2015.
Kikao cha Mawaziri, kinachoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Zimbabwe, Mhe. Dkt. Simbarashe Mumbengegwi, kinatayarisha agenda ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi, ambao utajikita kwenye Mpango Mkakati wa Maendeleo ya Viwanda wa nchi za SADC. Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal, anatarajiwa kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kwenye mkutano huo, utakaofanyika chini ya Mwenyekiti wa SADC, Rais Robert Mugabe.
Katika kikao cha Mawaziri, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe, anawakilishwa na Naibu wake, Mhe. Dkt. Mahadhi Juma Maalim, ambaye aliwasili Harare jana. Washiriki wengine ni Waziri wa  Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Abdallah Kigoda, Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mwigulu Nchemba, Naibu waziri wa Uchukuzi, Mhe. Dkt. Charles Tizeba na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Gerson Lwenge.
Mbali na mkakati wa maendeleo ya viwanda na mpango wa utekelezaji wake, Mawaziri watajadili Mpango wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Miundombinu na uanzishwaji wa Soko Huria la Utatu baina ya nchi za SADC, EAC na COMESA.
Kikao cha Mawaziri kilitanguliwa na Kikao cha Maafisa Waandamizi, kilichosimamiwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Rajab Gamaha na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Musa Uledi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Zimbabwe, Mhe, Simbarashe Mumbengegwi akifungua Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) unaojadili Mkakati na Mwongozo wa kuelekea Maendeleo ya Viwanda katika Kanda ya SADC. Mhe. Mumbengegwi amefungua mkutano huo jijini Harare, Zimbabwe  huku akiwa na huzuni kubwa kufuatia taarifa ya kifo cha Bregedia Jenereli Hashim Mbita ambaye alitoa mchango mkubwa katika ukombozi  wa nchi za Kusini mwa Afrika. Mhe. Mumbengegwi aliwaomba wajumbe wote wa mkutano kusimama ili kumuombea dua Bregedia Hashim Mbita.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda (Mb) wa katikati akiomba dua kumkumbuka Brigedia Hashim Mbita. Kulia kwa Mhe, Kigoda ni Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mwigulu Nchemba (Mb) na kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Dkt. Mahadhi Juma Maalim (Mb) nao pia wakimuombea dua Brigedia Jenerali Hashim Mbita.
Meza kuu nayo ikimuombea  Brigedia Jenerali Hashim Mbita. Kwa habari zaidi na picha BOFYA HAPA 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Nawakumbusha kutoa walau msimamo kuhusu ishu ya sauzi, naijeria wameonesha kuchukizwa na wamekataa kunyamaza.....kama mbwai mbwai tu.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...