Na. Leonard Mwakalebela, Norway
 
UJENZI wa mtambo wa kuchakata gesi asili kwa ajili ya matumizi mbalimbali (LNG) mjini Mtwara unakadiriwa kuchukua miaka takriban saba.

Meneja Uendeshaji wa kampuni ya Statoil Tanzania Bw. Thomas Mannes amesema kuwa, mambo yakienda kama yalivyopangwa, mtambo huo utakuwa tayari kwa uchakataji kati ya mwaka 2022 au 2023.

Akizungumza na viongozi wa dini wa Tanzania waliotembelea mtambo wa uchakataji gesi wa Statoil uliopo Karsto, Bw.Mannes amesema kuwa mradi huo mkubwa utagharimu mabilioni ya dola za Marekani.

"Tunakadiria itachukua kama miaka saba, mmoja kwa utafiti wa eneo kujua uimara wake kiufundi, miaka miwili ya utafiti wa kiuhandisi na michoro na miaka minne ya ujenzi wenyewe" alisema. Kwa mujibu wa Bw. Mannes,tayari wameishapendekeza maeneo yanayofaa kwa ujenzi wa mtambo huo na hivi sasa wabia wa mradi wanateua timu ya pamoja itakayosimamia mradi huo.

Mradi huo utakuwa wa pamoja kati ya Shirika la Maendeleo ya Mafuta nchini (TPDC) na kampuni za Statoil, BG, ExxonMobil, Ophir na Pavilion. Mradi huo utaenda sambamba na miradi mingine ya mafuta ya vitalu 1,3 na 4 inayoshirikisha TPDC, BG,Ophir na Pavilion na mradi wa gesi wa kitalu 2 wenye ubia kati ya TPDC, Statoil na ExxonMobil.

Bw. Mannes alieleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutakuwa na manufaamakubwa kwa Tanzania kwani kutoongeza mapato na nafsi za ajira, kutachochea biashara za bidhaa na huduma, kutoongeza mchango katika Pato la Ndani la Taifa (GDP) na kutaleta uwiano mzuri wa biashara.

Aidha amewataka Watanzania hususani wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara kujipanga izuri kwa ajili ya kufanya biashara ya bidhaa na huduma kwani kampuni yake itatoa kipaumbele wa kufanya biashara na wazawa.
Bw. Mannes aliongeza kuwa mkataba kati ya Statoil na serikali ni wa manufaa kwa pande zote mbili na kuwa ni wa viwango na taratibu zote za kimataifa. Naye Meneja Mawasiliano wa kampuni hiyo Bw. Ove Tungesvik alisema kuwa mtambo wa Karsto ndio mkubwa kuliko yote barani Ulaya.

Kwa upande wao, viongozi hao wa dini wameishauri kampuni ya Statoil kuwajengea uwezo watanzania, kupitia mafunzo na programu nyingine, kama Wanorway walivyosaidiwa na wamarekani katika miaka ya 1970, ili watanzania nao waweze kuisimamia sekta ndogo ya mafuta na gesi katika miaka michache ijayo.

Viongozi hao wa dini wapo mjini Stavanger, nchini Norway katika ziara ya mafunzo ya sekta ndogo ya mafuta na gesi. Ziara hiyo imeandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na Serikali ya Norway kupitia kwa Ubalozi wa Norway nchini Tanzania.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Du miaka 7 ? Mwanangu si atakua kashamaliza shule

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...