Rais Dkt. Jakaya Kikwete na Mwenyekiti wa China National Offshore Oil Corporation Bwana Wang Yilin wakizindua rasmi mtambo mpya wa utafutaji wa mafuta na gesi baharini, Uzinduzi huo ulifanyika kwenye Makao Makuu ya Shirika hilo huko Beijing tarehe 22.10.2014.
 Rais Dkt. Jakaya Kikwete akiongoza ujumbe wa Tanzania unaozuru nchini China wakiangalia vifaa mbalimbali vinavyotumiwa na Shirika la  CNOOC la China katika kazi ya utafutaji wa mafuta na gesi baharini wakati walipotembelea Makao Makuu ya Shirika hilo huko Beijing tarehe 22.10.2014.
 Rais Dkt. Jakaya Kikwete akishirikiana na Mkewe Mama Salma Kikwete na Professa Li Songshan (kushoto kwa Rais Kikwete), Mwanzilishi wa Kijiji cha Sanaa cha Afrika kuondoa kitambaa ikiwa ni ishara ya kufungua rasmi kijiji hicho kilichopo katika wilaya ya Songzhuang nchini China tarehe 22.10.2014.

JK: Mfumo wa Rais kung’atuka madarakani ni mzuri
. Unatoa nafasi kwa nchi kupata mawazo na fikra mpya
.Anaamini Tanzania itapata Rais bora zaidi wa kumrithi yeye
. Atamani muda wake umalizike akalee wajukuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa mfumo wa Tanzania ambako Rais anatumikia nafasi ya uongozi kwa muhula wa miaka mitano na siyo zaidi ya miaka 10 ni mfumo mzuri na unaovutia kwa sababu unaiwezesha nchi kupata fikra na mawazo mapya.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa anaamini kuwa Tanzania itapata Rais bora zaidi kuliko yeye, Rais ambaye ataiwezesha Tanzania kusonga mbele kwa kasi kubwa zaidi.
Rais Kikwete pia amesema kuwa anayo hamu kubwa ya kumaliza muda wake wa uongozi, ili arudi kijijini kushughulika na wajuu wake na mifugo yake.
Rais Kikwete ametoa kauli hiyo leo, Jumatano, Oktoba 22, 2014, mjini Beijing, China, wakati akizungumza na mabalozi wa Afrika wanaoziwakilisha nchi zao katika China.
Mkutano huo uliofanyika kwenye Nyumba ya Kufikia Wageni wa Serikali ya China ya Diaoyutai, ulikuwa shughuli ya kwanza ya Rais Kikwete katika ziara yake rasmi ya siku sita ya Jamhuri ya Watu wa China ambako amealikwa na Rais Xi Jinping.
Wakati wa maswali na majibu, Mheshimiwa Balozi Sola Onadipe, Naibu Balozi wa Nigeria katika China, alishangazwa na kauli ya Rais Kikwete kuwa anatamani amalize muda wake wa uongozi, ili astaafu na kusema kuwa lingekuwa jambo la maana  kwa Afrika kama viongozi wengine wangekuwa na mawazo ya namna hiyo ya kuheshimu Katiba za nchi zao na kung’atuka kwenye uongozi muda wao unapowadia.
Rais Kikwete amemwambia Balozi huyo: ” Ni kweli naona kama muda hauendi kwa kasi ya kutosha, ili niweze kuwa raia wa kawaida na nipate muda wa kuchunga ng’ombe na mbuzi wangu na nilime mananasi yangu kwa nafasi ya kutosha. Lakini Mheshimiwa Balozi usishangazwe na utayari wangu kuondoka katika uongozi.”
“Kwanza utaratibu huu wa miaka mitano ama miaka 10 ni utaratibu wa Kikatiba, ni jambo lililoko katika Katiba yetu na hatuna kishawishi cha kulibadilisha. Pili, kazi hii ya Urais ni kazi ngumu sana. Kwa hakika, binafsi nawaonea gele sana wenye nguvu na ubavu wa kutaka kubakia kwenye kazi hii kwa miaka mingi. Pengine wana nguvu zaidi kuliko mimi,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“ Lakini pia kuna uzuri katika mfumo huu wa kwetu kwa sababu kila baada ya miaka mitano na hata kama ni baada ya kila miaka kumi, anaingia mtu mwingine madarakani akiwa na fikra mpya na mawazo mapya.”
“ Mfumo huu ni mfumo unaoniridhisha sana na wala hakuna kinachonishawishi nibakie katika madaraka zaidi ya muda wangu kikatiba. Nina hakika, nchi yetu itapata kiongozi mwingine, bora kuliko hata mimi, kuongoza vizuri nchi yetu.”
Rais Kikwete pia amesema kuwa siyo busara pia kwa kiongozi kuwasikiliza wale wanaoshauri wakisema kuwa akiondoka madarakani nchi itavurugika.
“Kwa hakika, hawa wanatetea maslahi yao tu wakisema kuwa ukiondoka wewe madarakani, wao hawatakuwa tena mabalozi ama mawaziri ama nafasi nyingine yoyote.”

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

22 Oktoba, 2014



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Sijapendezwa na kauli ya Raisi wetu...hapo ni sawa na kutukejeli sisi wananchi wa kawaida tunaohangaika kucha kutwa na ngombe, mbuzu na kulima mananasi!

    Hivi haukutambua hilo tangu ungali kijana? umekalia siasa tangu enzi hizo za ujana wako leo ndio unakumbuka kilimo cha mananasi na kuchunga ngombe na mbuzi??

    kwa nini uligombea kipindi cha pili kama nia yako sio kuihujumu nchi sasa umevuna sana ndio unatoa kejeli! ungesema hivi kabla hujaingia madarakani!!

    kaa kimya acha uswahili wako, tumika kama ulivyoomba wananchi, muda ukifika ndio ukajibebe mwenyewe kama ni kuchunga ama kulia ama kuvua samaki!!

    Tena usiingilie tena maswala ya uongozi....ukafanye hayo unayotamani kwenda kuyafanya!!!!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...