MAKAMPUNI ya Songas Tanzania na Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ni makampuni pekee ya binafsi yazalishayo umeme ambayo kwa sasa uzalisha umeme kwa ajili ya gridi ya Taifa wakati mengine yaliyobaki Aggreko na Symbion Power Tanzania yakiwa yanatumika tu wakati wa dharura. 

Uwezo ulioongezwa katika mitambo ya gesi asilia ya Songas iliyopo Ubungo ni ya megawati 189, wakati kampuni ya IPTL inatumia mafuta mazito na uwezo wake ni kuzalisha megawati 103, ingawa uzalishaji huo ubadilika mara kwa mara kutokana na mahitaji katika gridi ya Taifa. 

Kaimu Meneja Uhusiano wa Tanesco, Bw. Adrian Severin alisema hii ni kutokana na ukweli kuwa  nchi kwa sasa inazalisha umeme kutoka katika vyanzo vingine vyenye gharama nafuu ambavyo ni maji na nishati ya mvuke (thermal power).
“Mitambo ya uzalishaji umeme kupitia maji kwa sasa inazalisha kati ya megawati 450 hadi 500 toka katika mitambo yenye uwezo wa megawati 561.84 wakati mitambo mitatu ya gesi inayomilikiwa na Tanesco katika eneo la Ubungo na Tegeta inazalisha jumla ya megawati 252. 

“Hii inafanya jumla ya uzalishaji kutokana na maji na nishati ya mvuke kuwa megawati 752 ambayo inatosheleza mahitaji katika gridi ya taifa. Mahitaji makubwa ya umeme Tanzania mara ya mwisho yalirekodiwa kuwa megawati 898.5,” alibainisha Bw. Severin. 

Uzalishaji wa pamoja kwa Symbion ni megawati 120 ambapo uzalisha megawati 60 toka katika mafuta aina ya Jet – 1 na nyingine  megawati 60 kupitia gesi asilia, wakati Aggreko inazalisha megawati 100 kwa kutumia mafuta mazito katika mitambo yake iliyopo Ubungo na Tegeta jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, Bw. Severin alisema kuwa mitambo ya Symbion na Aggreko kwa sasa itatumika tu katika hali ya dharura itakapotokea.

“Katika hali ambayo kina cha maji katika mitambo yetu inayozalisha nishati kupitia maji kimepungua au pale ambapo mitambo yetu inayozalisha nishati ya mvuke inafanyiwa ukarabati, uwa mara nyingi tunawaomba Aggreko na Symbion kuingiza umemewao katika gridi ya taifa ili pasiwepo na adha ya mgao,” Alisema Bw. Severin.  

Akizungumza kwa njia ya simu jana juu ya kwa nini anadhani kampuni yake inaendelea kuzalisha umeme katika gridi ya Taifa, licha ya mitambo yake kutumia mafuta mazito ambayo imeongeza gharama za uzalishaji, Mwenyekiti Mtendaji wa IPTL, Bw. Harbinder Sethi alisema IPTL chini ya uongozi wa Pan Africa Power Solutions (PAP) imejitoa katika hali ya kupata faida kubwa ya kupindukia, kwa kuanza kufanya uendeshaji wa gharama nafuu ikiwa na lengo la kuipatia nchi (wateja) umeme wa bei nafuu. 

“Ni kweli kuwa uzalishaji wa nishati kwa kutumia mafuta mazito ni ghali na ndiyo sababu tuna mpango wa kuweka mitambo ya gesi ya megawati 200 pembezoni mwa IPTL katika awamu ya kwanza ya mkakati wetu wa upanuzi. Majadiliano yanaendelea na mamlaka zote zinazohusika. Lengo ni kuhakikisha kuwa watanzania wote wanapata nishati ya bei rahisi katika ukanda wa Afrika mashariki na kati na kuwafikia watu wengi zaidi hivi karibuni,” alisema. 

Bw. Sethi alionyesha kuwa na matarajio kwamba mabadiliko yaliyoletwa na PAP ndani ya IPTL, itaisaidia kampuni hiyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kuleta mabadiliko ya hali ya umeme iliyopo na unafuu wa gharama zake nchini. 

Vyanzo vya nishati kupitia nguvu ya maji nchini ni pamoja na Kidatu megawati 204, Kihansi megawati 180, Mtera megawati 80, Nyumba ya Mungu megawati 8, New Pangani megawati 68 na vile vile Hale megawati 21.  

Kwa upande mwingine, Tanesco inaendesha mitambo miwili ya gesi iliyopo Ubungo kwa pamoja ikizalisha umeme wa megawati 207 pamoja na mtambo mmoja wa gesi uliopo Tegata wenye uwezo wa kuzalisha megawati 45 na mtambo mwingine ukitumia mafuta ghafi mazito uliopo Nyakato, Mwanza wenye uwezo wa kuzalisha megawati 63. 
 Mafundi wakiwa kazini katika chumba cha Independent Power Tanzania Limited (IPTL) cha uendeshaji mitambo.  
 Moja kati ya karakana za kampuni ya ufuaji umeme za IPTL.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...